Powered By Blogger

Thursday, September 27, 2012

MFAHAMU SHARO MILIONEA

Sharo katika pozi


UNAPOZUNGUMZIA tathinia ya filamu hapa nchini huwezi kulisahau jina la Hussein Mkieta ambaye amekuwa midomoni mwa watu wengi kutokana na ustadi mkubwa wa kuigiza hususan vichekesho.

Mkieta kama anavyofahamika na wengi kwa jina la Sharomilionea ni kijana mtanashati ambaye nyota yake inazidi kungara siku hadi.

Katika miaka ya hivi karibuni tasnia ya maigizo hususan vichekesho imekuwa kwa kasi kubwa ba hilo limeendana sambamba na kuibuka kwa vipaji vipya katika sanaa hiyo.

Sharomilionea ni miongoni mwa wasanii wa vichekesho ambao wanazidi kujizolea umaarufu na sifa kemkem kutokana na umahiri wake wa kutoa burudani ikihusisha sanaa ya vichekesho pamoja na muziki wa kizazi kipya.

Mkiet amefanikiwa kuteka nyoyo za mashabiki na wapenzi wengi wa vichekesho kutokana na umahiri huo ambao hivi sasa anazidi kuteka soko la sanaa hapa nchini.

Msanii huyo ambaye mashabiki wake wengi ni vijana na watoto pamoja na wazee amekuwa akibuni staili mbalimbali kuvutia mashabiki wake hususdan kwa kutia madoido ya Kimagharibi na kujiweka katika maisha ya juu katika uigizaji wake.

“Niliamua kuwa mbunifu ili kutafuta staili tofauti na wachekeshaji wengine na ninashukuru hilo limeweza kufanikiwa na sidhani kama kuna mtu anaweza kunifikia kwa sasa," anasema mchekeshaji huyo.

Msanii huyo ambaye amekuwa akishirikiana bega kwa bega na mchekeshaji maarufu hapa nchini Amri Athuman 'King Majuto' anaweka wazi kwamba ingawa anapenda kuigiza maisha ya juu binafsi hapendi kuishi maisha ya aina hiyo.

"Niko tofauti sana na vile jamii inavyoniona kupitia maigizo yangu...huwa sipendi kuishi maisha kama yale ila pale nipo kazini ndio maana ninaonekana vile," anasema.

Anasema lengo lake la kuigiza staili ya aina ile ni kuwafundisha wenye tabia kama hizo kuacha kwani binadamu wote ni sawa na hakuna aliyebora kuliko mwingine.

Mkiet anasema kuna baadhi ya watu katika jamii wanapokuwa na maisha tofauti na watu wengine hupenda kujionyesha na kuwadharau wenzao ambao maisha yao ni yakawaida na kwamba jambo hilohalipendi katika  maisha yake.

“Binafsi siishi maisha yale na wala siyapendi kabisa maana nawaonyesha ili waweze kuachana na tabia hizo kwa kuwa hazina maana yoyote  zaidi ya kuonyesha ni jinsi gani walivyokuwa malimbukeni kuiga maisha ya watu wa Magharibi”anasema.

Kwa mujibu wa Mchekeshaji huyo, anakiri kwamba asingeweza kufikia hapo alipo sasa bila ya kumsahau Mzee Majuto ambaye amemfundisha mambo mengi ya sanaa.

Anasema Mzee Majuto amemsaidia kwa kiasi kikubwa kufikia hapo alipo na kamwe hawezi kusahau mchango wake katika tathinia ya sanaa hapa nchini.

"Ninawashukuru wasanii wenzangu wote ambao kwa namna moja ama nyingine wamenipa msaada mkubwa hadi kufikia hapa nilipo...Mzee Majuto ni jembe langu ambalo siwezi kulisahau katika maisha yangu yote ," anasema.

Mkiet licha ya kujikita katika sanaa ya vichekesho lakini anajihusisha na muziki wa kizazi kipya ambapo pia ameonyesha kiwango cha hali ya juu kutokana na staili ya uimbaji wake.

Miongoni mwa nyimbo alizoziachia hewani msanii huyo ni pamoja na Sondela na Hawataki alioshirikiana na Rich Mavoko pamoja na Kanali Top zimefanikiwa kumuweka katika nafasi nzuri katika chati za muziki.

Anasema aliamua kujikita katika muziki kwa ajili ya kujitafutia riziki na si vyenginevyo na kuongeza kuwa hakuingia kwenye muziki kupahatisha bali amedhamiria kufanya kweli kwenye tathinia hiyo.

Historia ya mchekeshaji huyo, inaonyesha alianza kujikita katika sanaa tangu akiwa shule ya msingi Tanga na alipomaliza alifanikiwa kuja Dar es Salaam na hapo kipaji chake kilizidi kukua na kujipatia umaarufu baada ya kukutana na muigizaji mkongwe Mzee Majuto na kujiingiza moja kwa moja katika Vituko Show.

Baadhi ya filamu alizoshiriki mchekeshaji huyo kwa kushirikiana na Mzee Majuto na wasanii wengine ni pamoja na Chuma Ulete, Pedeshee, Vyumba vimejaa na Kozi Man.