Powered By Blogger

Sunday, September 30, 2012

YAFAHAMU MAISHA YA ROMARIO KIMZIKI

ROMAN MNG'ANDE 'ROMARIO'


UNAPOIZUNGUMZIA bendi ya Msondo Ngoma 'Baba ya muziki' huwezi kumsahau Romani Mng'ande 'Romario', kutokana na umahiri wake wa kupuliza tarumbeta.

Mng'ande, ni msanii mwenye historia kubwa na aliyejipatia umaarufu mkubwa katika historia ya muziki wa nchi hii.

Umaarufu wa msanii huyo, haukuja hivi hivi bali ulitokana na mambo mbalimbali ikiwemo vituko na vichekesho vingi anavyofanya akiwa kwenye kazi yake hiyo.

Msanii huyo, amekuwa masikioni mwa mashabiki wengi hususan wapenzi wa muziki wa dansi kutokana na mbwembwe zake.

Akizungumza juzi, Mng'ande, anaanza kuizungumzia historia yake kimuziki ambapo anasema alianza kujiingiza kwenye bahari hiyo mwaka 1973 akiwa katika kundi la Father Kanuti, mkoani Morogoro.

Anasema akiwa kwenye kundi hilo, alianza kwa kupiga vyombo mbalimbali ikiwemo tarumbeta ambalo anauzoefu nalo mkubwa.

Mng'ande, anasema katika kundi hilo, alidumu kwa miaka sita ambapo mwaka 1979 alijiunga na kundi la Urafiki Jazz lililokuwa na masikani yake jijini Dar es Salaam.

Anasema kilichomsukuma kujiunga na kundi la Urafiki kipindi hicho ni kukuza kipaji chake cha muziki na kujipatia ukomavu.

Mng'ande, ambaye anasifika kwa vituko na tambo za kila aina, anasema katika kundi hilo hakuweza kudumu kwa muda mrefu kutokana na kuhitajika katika kundi la Tanzania Stars Magosi.

Anasema mara kwa mara viongozi wa bendi hiyo, walikuwa wakimfuata ili aweze kujiunga nalo na kuiongezea nguvu bendi hiyo.

Msanii huyo, anasema mwaka 1981 uongozi wa Tanzania Stars Magosi, ulifanikiwa kumuhamisha katika bendi ya Urafiki, baada ya kumpandia dau.

"Unajua sisi wasanii ni kama vile wachezaji mpira mtu akikupandia dau huwezi kuliacha lazima umfuate...tunafanya mziki ili tupate hela sasa kama umepewa hela utaweza kuziacha.

"Ndio maana hata nilipofuatwa na viongozi wa Tanzania Magosi sikuweza kukataa kwani niliangalia maslahi mbele mambo mengine badae," anasema.

Anasema mwaka 1983, alidumu katika bendi hiyo na alifanikiwa kujiongezea umaarufu na kuanza kusikika masikioni mwa mashabiki wengi.

Mng'ande ambaye ni baba wa watoto wanne, anasema hata hivyo, hakuweza kudumu kwa muda mrefu katika bendi hiyo na akaanza kufuatwa na viongozi wa Juwata Jazz kipindi hicho sasa Msondo Ngoma.

"Kama unavyojua nyota njema huonekana asubuhi na ndivyo ilivyoanza kungara kwangu...historia yangu ya muziki ni ndefu lakini inaonyesha jinsi nilivyoanza kufanikiwa," anasema.

Anasema baada ya kufuatwa na viongozi wa Juwata na kuonyesha nia ya kutaka kumchukua kwenye kundi hilo, hakufanya kosa na aliwaambia milango iko wazi.

"Lengo langu lilikuwa kuimba kwenye bendi kubwa kama Juwata, hivyo nilipofuatwa sikufanya kosa nikawaambia milango iko wazi waje tuzungumze.

"Kwa kweli viongozi wale hawakusita walinifuata na kunieleza dhamira yao ni kutaka nijiunge na bendi ile ambayo kipindi hicho ilikuwa moto wa kuotea mbalimbali," anasema.

Anasema mwaka 1983, alijiunga rasmi na bendi ya Juwata Jazz, wakati huo ikiwa na waimbaji mahiri akiwemo marehemu TX Moshi William, Said Mabera na wengine wengi.

Mng'ande, anasema tokea kipindo hicho hadi sasa hajatoka kwenye bendi hiyo wala hafikirii kutoka mpaka atakapoamua kuachana na muziki.

"Kama nilirogwa basi viongozi wa Juwata walipata mganga kwani tokea nilipojiunga na bendi hiyo hadi sasa sijatoka wala sifikirii kutoka hata iweje.

"Nimepata mafanikio makubwa nikiwa katika bendi hiyo na imenisaidia kufahamiana na watu wengi, viongozi wa serikali, kwa kweli nimepata mafanikio makubwa katika maisha yangu.

"Siwezi kusita kuwa bendi ya Msondo, imenitoa kimaisha, imenifanya kiwango changu cha muzimki kukua siku hadi siku, siwezi kuisahau katika maisha yangu yote," anasema.

Anasema baada ya kupata mafanikio mengi katika bendi hiyo, anafikiria kujenga maisha yake ili aweze kuishi vizuri na familia yake.

Mng'ande, anasema hana mpango wa kuanzisha bendi na lengo lake ni kuzidi kujiimarisha katika kazi yake hiyo ili bendi yake iweze kufanya vyema.

Anasema katika maisha yake ya muziki hawezi kumsahau marehemu TX Moshi kwani alikuwa rafiki yake mkubwa na alikuwa akimshauri mambo mengi.

Romario, anasema waimbaji wengine ambao hawezi kuwasahau ni pamoja na Said Mabera na Muhidini Ngurumo.

Anasema wimbo ambao hawezi kuusahau ni kibao cha 'Isikutonza iyudi chaum' uliotungwa na marehemu Mwanjiro na alishiriki kwa kiasi kikubwa kupiga vyombo katika wimbo huo.

"Huu wimbo ukipigwa hata niwe wapi lazima ni simame kidogo niusikilize, naupenda sana kuliko wimbo mwingine, nilishirikishwa kuupiga," anajigamba.

Msanii huyo ambaye amesoma katika shule ya sekondari Kingurunyembe, Morogoro anasema albamu za Msondo ambazo hawezi kuzisahau ni pamoja na Mwanaume tumeumbwa mateso, Kilio cha mtu mzima.

Romario mbali na kipaji cha kupuliza tarumbgeta lakini amejaaliwa kipaji cha uimbaji ambapo mara nyingi ameonekana akiimba nyimbo mbalimbali.