Powered By Blogger

Thursday, September 27, 2012

ASEMAVYO JOKHA KASIMU

GWIJI WA MIPASHO JOKHA KASIMU


"KUPIGANA vijembe katika taarab hakukuanza leo wa jana, tokea enzi za marehemu Leila Khatib na Khadija Kopa walikuwa wanapigana vijembe.

"Sisi waimbaji chipukizi tumerithi kutoka kwao...siwezi kushangaa kusikia mtu anampiga vijembe mwenzake kupitia tasnia hii," anasema Jokha Kassim, muimbaji mahiri wa taarab anayeimbia kundi la Tanzania Moto.

Anasema amelazimika kulizungumzia hilo, abaada ya kuwepo tetesi kuwa muimbaji huyo mwenye sauti ya kuvutia kuwa nyimbo zake nyingi zimekuwa zikimlenga kiongozi wa Jahazi, Mzee Yussuf na mke wake Leila Rashid.

Jokha, ambaye alikuwa mke wa kwanza wa Yussuf na kubahatika kupata mtoto mmoja anayeitwa Yussuf, tangu walipoachana kumekuwa na minong'ono kuwa muimbaji huyo amekuwa akiimba nyimbo za mafumbo na kumpiga vijembe mtalaka wake huyo.

Akizungumza hivi karibuni, Jokha anaanza kwa kusema muziki ni malumbano na mambo ya kujibizana kupitia fani hiyo imeanza zamani.

Anasema anakumbuka tangu akiwa mdogo, waimbaji walikuwa wakijibizana kupitia tasnia hiyo na haoni ajabu sasa waimbaji kuendelea kujibizana kupitia muziki.

"Nakumbuka marehemu Leila Khatibu na Khadija Kopa walivyokuwa wakipigana vijimbe wala lengo lao halikuwa baya ilikuwa ni kuvuta mashabiki.

Hata hivyo, muimbaji huyo, anasema si kweli kama nyimbo zake anazoimba zinalenga kuwapiga vijembe Yussuf na Leila na kwamba anafikisha ujumbe kwa jamii husika.

Anasema majibizano kwenye muziki ni vitu vya kawaida na hashangazwi waimbaji kujibizana kwani kunaleta changamoto nyingi.

Jokha, anayetamba na kibao cha domo la udaku, alioutoa hivi karibuni anasema hakumlenga mtu katika wimbo huo.

Anasema mpangilio wa mashairi yanayopatikana kwenye wimbo huo, yamekuwa yakileta tafsiri mbaya kwenye jamii ambao wengi wanadhani alimlenga mtu.

Jokha, anasema wimbo huo haukumlenga mtu yoyote bali ulingela kuielimisha jamii mambo mbalimbali yanayotokea.

Anasema hivi sasa anajiandaa kuachia kibao chengine anachoamini kuwa kutakuwa moto wa kuotea mbali.

Akizungumzia maisha yake ya muziki hivi sasa tangu alipojiunga na kundi la T. Motto, anasema mambo yanakwenda vizuri na kipaji chake kinazidi kukua.

Anasema akiwa katika kundi hilo, wamebahatika kurikodi albamu inayoitwa 'Aliyeniumba hajanikosea' ambayo ilikuwa gunzo la jiji.

Jokha, anasema hivi sasa wako mbioni kupakua albamu mbili kwa mpigo, ambazo ni Mimi staa na Domo la udaku.

Anasema baadhi ya nyimbo katika albamu hizo zimekamilika na amezitaja kuwa ni pamoja na mwanamke hashuo, domo la udaku, mimi staa na wewe si daktari wa mapenzi.

Jokha, anasema wako katika hatua za mwisho kwa ajili ya uzinduzi wa albamu hizo na tayari baadhi ya nyimbo hizo wameshaanza kuwasikilizisha mashabiki wao.

Anamalizia kwa kuwaomba wapenzi na mashabiki wake wake mkao wa kula kuzipokea albamu hizo na anawaomba mashabiki wake wategeme mambo mazuri kutoka kwake.