'mtoto wa mfalme' Abubakar Sudi 'Amigo'
"NAMKUBALI sana Mwinjuma Muumini 'Kocha wa duniani' ndiye aliyenifanya niingiye kwenye tasnia hii na kufika hapa nilipo.
"Nyimbo zake za Tunda na Kilio cha yatima, nilikuwa nikizihusudu sana na kila nilipokuwa nazisikia nilitamani siku moja niwe kama yeye," ndivyo alivyanza mazungumzo yake Abubakari Sudi 'Amigo'.
Amigo ambaye hivi sasa amekuwa midomoni mwa mashabiki wengi hususan wa muziki wa taarab kutokana na umahiri wake wa uimbaji.
Miongoni mwa mambo yanayosababisha mashabiki wamkubali muimbaji huyo anayeimbia kundi la Jahazi Morden Taarab ni baada ya kuachia wimbo unaoitwa Full shangwe ambao umekuwa gunzo la jiji hivi sasa.
Akizungumza mwishoni mwa wiki, Amigo alisema alijiunga na Jahazi mwishoni mwa mwaka 2009 akitokea katika kundi la East Afrika Melody 'Watoto wa mjini'.
Alisema baada ya kuingia mkataba na Jahazi chini ya Mkiurugenzi wake, Mfalme Mzee Yussuf, alipewa wimbo unaoitwa Domo kaya.
Amigo, ambaye mara nyingi mashabiki wanamuitwa 'Mtoto wa Mfalme' anasema wimbo huo ulianza kumpatia umaarufu mkubwa.
Alisema baada ya kuonekana kufanya vizuri katika wimbo huo uliokuwa kwenye albamu ya Daktari wa Mapenzi, ndipo Yussuf alipohamasika kumpatia wimbo wa Full shangwe ambao hivi sasa umekuwa gumzo la jiji.
Amigo, anakiri kwamba wimbo wa Full shangwe umemfanya awe midomoni mwa mashabiki wengi wa taarab hivi sasa na daima atamshukuru Yussuf kwa kumtungia kibao hicho.
"Katika hili sina budi nimshukuru sana Mzee Yussuf kwa kunifanya nifike hapa nilipo, baada ya kunitungia wimbo wa Full shangwe umeniongezea umaarufu mkubwa.
"Kupitia kwa Mzee kumenifanya ningara kimaisha na kimuziki, ni mtu ambaye amejaaliwa roho ya pekee yake na Mungu tofauti na viongozi wengine wa bendi wenye roho za kwanini," alisema.
Alisema kwa sasa hana mpango wa kulihama kundi la Jahazi na kwamba anachokifanya ni kuongeza juhudi ili aweze kufikia lengo alililojiwekea kimuziki.
Muimbaji huyo mwenye umbo dogo, alisema lengo lake ni kuvaa viatu vya Yussuf ili awe muimbaji bora, mtungaji na mpigaji.
Alisema ushirikiano uliopo baina ya waimbaji wa Jahazi na viongozi wa kundi hilo ndio uliomfanya awe juu kimuziki.
Muimbaji huyo alisema kabla hajajiingiza kwenye muziki alikuwa akimuhusudu sana Mwinjuma Muumini 'Kocha wav duniani' na ndie aliyesababisha ajiingize kwenye muziki.
HISTORIA YAKE KATIKA MUZIKI.
Amigo, alisema alianza rasmi kujiingiza kwenye muziki mwishoni mwa mwaka 2004.
Alisema kipindi hicho alianzia kwenye kundi la muziki wa kizazi kipya lililofahamika kama Karama's Camp na akiwa katika kundi hilo alibahatika kuimba nyimbo mbili ambazo ni Sina mwengine na Nimefanyaje.
Kwa mujibu wa muimbaji huyo, kundi la Karama's Camp lilianzisha kundi lingine la Segere ambapo alikuwa akiimba nyimbo tofauti tofauti.
Alisema baada ya mudi kundi hilo lilipanuka na kuanzisha lingine lililofahamika kama East rusha roho.
Muimbaji huyo, alisema mwaka 2008 alijiunga na kundi la East Afrika Melody, ambapo alibahatika kuimba wimbo unaoitwa Ilove U, ambapo mwishoni mwa 2009 alijiunga na Jahazi.
MATARAJIO YAKE.
Amigo, alisema anatarajia kucheza filamu ambapo hivi sasa tayari ameshatayarisha filamu inayofahamika kama Ladha ya Maharage.
Alisema filamu hiyo imewashirikisha wakongwe wa filamu hapa nchini akiwemo Dk. Cheni, Sebe, Riami na wengine wengi. Amigo, alisema filamu hiyo iko jikoni na inatarajiwa kupakuliwa muda wowote kutoka sasa.
Alisema kipaji cha uigizaji anacho muda mrefu na alishawahi kupata mafunzo kwa ajili ya kuendeleza kipaji hicho.
Amigo, alisema pamoja na kuimba taarab hivi sasa lakini anatarajia kuimba muziki wa kizazi kipya kuendeleza kipaji chake.
Alimazilizia mazungumzo yake kwa kusema, alimaliza darasa la saba katika shule ya Msingi Makumbusho mwaka 1999 na mwaka 2000-2003 alimaliza kidato cha nne katika shule ya Sekondari ya Al-haramaini, zote za Dar es Salaam.