Powered By Blogger

Sunday, October 21, 2012

MFAHAMU KIBAKULI

KIBAKULI

"Muhogo Mchungu ni kama baba yangu mzazi, amenisaidia sana katika maisha yangu mpaka sasa anaendelea kunishauri mambo mengi.

"Nakumbuka hata marehemu baba yangu alimwambia Muhogo Mchungu ipo siku nitakuachia Kibakuli na hiyo ilikuwa kauli ya mwisho ya marehemu baba," ndivyo alivyoanza kueleza msanii chipukizi Sadiki Mberwa 'Kibakuli'.

Hakika jina la msanii huyo aliyeanza kuigiza na wakongwe wa sanaa hapa nchini si geni masikioni mwa wapenzi wengi wa filamu kutokana na vituko na tambo alizokuwa akionyesha wakati wa kuigiza.

Kibakuli alianza kusikika mwaka 1999 wakati huo akiwa na kundi la Kaole lililosheheni waigizaji wengi mahiri wakiwemo marehemu Mzee Kipara na Mzee Pwagu.

Mbali na wakongwe hao, wasanii wengine waliokuwa wakiunda kundi hilo ni pamoja na Muhogo Mchungu, Bistaa na Bitei.

Akizungumza hivi karibuni, Kibakuli alisema kazi ya sanaa na maigizo aliianza rasmi mwaka 1999 akiwa anasoma darasa la sita katika shule ya Msingi Ukombozi iliyopo Manzese, Dar es Salaam.

Alisema alianza na kundi la Kaole lililokuwa limesheheni wakongwe wengi wa maigizo hapa nchini.

Kibakuli, alisema wakati anajiunga na kundi hilo alikuwa hana kipaji chochote cha uigizaji na wala alikuwa hatarajii kuigiza katika maisha yake yote.

"Mpaka leo hii najiuliza jinsi nilivyoingia kwenye sanaa hii lakini sipati jibu, kwani nilikuwa sijui lolote kuhusu maigizo na hata pale shule nilikuwa si shiriki mchezo wowote ule," alisema.

Alisema baada ya kujiunga na kundi hilo, alishiriki filamu iliyokuwa ikifahamika kwa jina la Fukuto ambapo aliigiza kama mtoto wa Muhogo Mchungu.

Kibakuli, alisema anakumbuka katika filamu hiyo iliyopata umaarufu mkubwa, walishiriki wasanii wazoefu wengi akiwemo marehemu Mzee Kipara na Mzee Pwagu.

Alisema katika filamu hiyo Bistaa aliigiza kama mke wa Muhogo Mchungu na yeye alikuwa mama yake.

Kibakuli, alisema katika filamu hiyo Muhogo Mchungu alikuwa na mke mwingine ambaye ni Bitei.

Alisema nyota yake ya uigizaji ilianza kuonekana katika filamu hiyo ambayo ilipata kupendwa na wapenzi wengi wa filamu hapa nchini kutokana na kusheheni vituko mbalimbali.

Muigizaji huyo, ambaye ni mtoto wa mwisho kati ya watoto watano kwenye familia yao, alisema uzoefu wa uigizaji aliupata kwenye kundi hilo lililokuwa na mastaa kibao.

Alisema licha ya kujiunga na kundi hilo akiwa 'Mbumbumbu' lakini alipata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa viongozi na wasanii waliokuwa wakiunda kundi hilo.

Kibakuli, alisema alijifunza mambo mengi kutoka kwa wazee waliokuwa kwenye kundi hilo, akiwemo marehemu Mzee Kipara ambaye mara nyingi alikuwa akimfundisha mambo mengi ya kiusanii na kimaisha.

Alisema busara na hekima za wazee waliokuwa wakiunda kundi hilo la sanaa zilimfanya aweze kukubalika na mashabiki wengi wa filamu hapa nchini.

Kibakuli, alisema baada ya kushiriki filamu hiyo, alilipa kisogo kundi la Kaole na kuanza kufanya kazi pekee yake.

Alisema filamu yake ya mwisho kushiriki ni 'Ngoma yangu' ambayo haikufanya vizuri kwenye soko kutokana na sababu mbalimbali.

Akizungumzia matarajio yake sasa baada ya kuipa kisogo kazi ya uigizaji, Kibakuli alisema hivi sasa anafanya kazi ya utayarishaji filamu 'Produce'.

Alisema hivi karibu anatarajia kuachia wimbo wake wa taarab ambao ameutunga unaofahamika kwa jina la 'Nilikua naye' aliomshirikisha Bistaa.

Kibakuli, alinidokezea kuwa analengo la kufunga ndoa lakini bado kidogo na kwamba katika ujana wake hajawahi kupata mtoto.

Alisema maisha anayoishi ni ya kawaida sana tofauti na wasanii wengine na kwamba hadi sasa anaishi kwenye nyumba ya kupanga maeneo ya Mbezi kwa Msuguli, Dar es Salaam.

Kibakuli, alisema Muhogo Mchungu ni miongoni mwa watu ambao hawezi kuwasahau katika maisha yake yote kutokana na msaada mkubwa aliompatia.

Alisema amepata mafunzo ya Production katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na kwamba yuko mbioni kujenga nyumba yake huko Mbezi Kwa Msuguli.

Historia ya muigizaji huyo inaonyesha alizaliwa Machi 2, 1985 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Alianza shule ya msingi mwaka 1999 katika shule ya Ukombozi Manzese na mwaka 2001 alijiunga na shule ya Sekondari ya Mbezi High School.