Powered By Blogger

Sunday, October 21, 2012

HUYU NDIYE MFALME MZEE YUSSUF

'BIG DADDY' MZEE YUSSUF

UNAPOWAZUMGUMZIA waimbaji wa taarabu hivi sasa huwezi kuliacha jina la Mzee Yussuf, kutokana na mchango wake mkubwa kwenye tasinia hiyo ndani na nje ya nchi.

Yussuf, kiongozi wa kundi la Jahazi Morden Taarab, amejipatia umaarufu mkubwa, kutokana na umahiri wake wa utungaji mashairi, upigaji kinanda na uimbaji.

Muimbaji huyo, alianza kungara akiwa katika makundi ya Zanzibar Stars na East Afrika Melody, kuanzia mwaka 2000 mpaka 2006 alipoamua kuanzisha kundi lake la Jahazi.

Wimbo wake wa kwanza kuanza kumng'arisha muimbaji huyo mahiri wa taraba katika ukanda huu wa Afrika Mashariki ni 'Kipendacho roho hula nyama mbichi'.

Wimbo huo ulianza kumpatia muimbaji huyo umaarufu mkubwa kwenye angaza za muziki wa taarab na kuanzia hapo hadi sasa anaendelea kuwika.

Kuanzishwa kwa kundi hilo, ambalo ndio la kwanza kupiga muziki wa morden kuliyaangusha makundi mengine yaliyokuwa yakivuma kwa kipindi hicho, yakiwemo ya Melody, Zanzibar Stars, Muungano na TOT.

Baada ya kuanzisha kundi la Jahazi, Yussuf alisimama kidete kuhakikisha anatoa burudani inayowaridhisha mashabiki wake na kufanikiwa kuliteka soko la muziki huo.

Muimbaji huyo, ambaye anafahamika kama 'Mfalme' amefanikiwa kutoa albamu nane tangu kuanzisha kundi hilo hadi sasa na kwamba hivi karibu anatarajia kutoa albamu ya tisa.

Baadhi ya albamu hizo ni pamoja na Tupendane wabaya waulizane, Wagombanao ndio wapatanao, Mpenzi chokleti, Daktari wa mapenzi,  Two in one, My valentine na VIP.

Akizungumza juzi mjini Dar es Salaam, Yussuf anasema hivi karibuni anatarajia kuachia albamu mpya itakayaofahamika kama 'Wasi wasi wako ndio maradhi yako' ambayo itakua na nyimbo sita na kwamba baadhi ya nyimbo zimeanza kukamilika ukiwemo wa mgodi wa dhahabu.

Anasema akiwa mkurugenzi wa kundi hilo, amepania kufanya mabadiliko makubwa katika muziki wa taarab ndani na nje ya nchi ili kuwapa ladha tofauti mashabiki wake.

"Nimepania kufanya mabadiliko makubwa katika tasnia ya taarab, nitashirikiana na waimbaji wa kundi letu katika kulifanikisha hilo, tunawaomba mashabiki wake mkao wa kula.

"Jahazi tunataka tufanye kile wanachopenda mashabiki wetu...tunawaahidi mambo mengi mazuri na tutawapa mashabiki ladha tofauti tofauti," anasema.

Anasema baadhi ya nyimbo zilizomo katika albamu hiyo, zitaanza kusikika hivi karibuni na zitaiimbwa kwenye maonyesho yake mbalimbali ili mashabiki waweze kuzifahamu.

Kwa mujibu wa Big Daddy, mbali ya kipaji cha uimbaji, anauwezo mkubwa wa kupiga kinanda, kita la solo, na utungaji wa mashairi.

Anasema kipaji chake kikubwa ni upigaji kinanda na kwamba tangu alipoanza kujikita kwenye taarabu alianza kwa kupiga kinanda na gita.

Yussuf, anasema kibaji cha uimbaji na utungaji wa mashairi ni cha kuzaliwa na anaamini kwa sasa hakuna muimbaji anayeweza kumfikia.

"Vipaji nilivyonavyo ni vya kuzaliwa, niko tofauti na waimbaji wengine ambao wamedandia fanii hii ukubwani...huwezi kunifananisha na muimbaji mwingine yoyote kwa sasa," anasema.

Muimbaji huyo, ambaye amezaliwa kwenye familia ya wasanii, anasema amepata mafanikio mengi tangu alipoanzisha kundi lake la Jahazi hadi sasa.

Anataja mafanikio hayo kuwa ni pamoja na kumiliki maduka mawili likiwemo la nguo lililopo Magomeni na la kuuza mikanda ya nyimbo lililopo Kariakoo.

Yussuf, pamaoja na mambo mengine anasema kundi lake hivi sasa limeanzisha timu ya mpira wa miguu inayoitwa Jahazi FC na inatarajiwa kushiriki mashindano mbalimbali.

"Ukiangalia kundi letu limepiga hatua kubwa kwa kweli, ndio kundi pekee la muziki linalomiliki timu ya mpira wa miguu hapa nchini, haya ni mafanikio makubwa na tunamshukuru Mungu kwa kutuwezesha kufika hapa tulipo," anasema.

Anasema yuko mbioni kutoa albamu yake binafsi ambayo itaitwa 'Mtadumu naye' itakayokusanya nyimbo nyingi alizotoa kipindi cha nyuma na ameahidi kuitengeneza kwa ustadi mkubwa.

Yussuf, anasema mbali na albamu hiyo pia anatarajia kutengeneza filamu yake na kutoa nyimbo za mduara ambazo tayari ameanza kuziandaa.

"Kwa sasa natarajia kuachia albamu yangu binafsi ambayo itakusanya nyimbo zote nilizotoa kipindi cha nyuma, hii itakuwa na ubora wa hali ya juu na itakuwa tofauti na nyingine.

"Kama unavyofahamu nina vipaji vingi na nimekuwa mbunifu wa muziki...hivi karibuni nitaachia nyimbo zangu nilizoziimba kwa staili ya mduara na tayari nimeshazianda," anasema.

Anasema anaishi maisha ya kawaida na ni tofauti na watu wanavyodhani kama anaishi maisha ya kifalme kama anavyofahamika.

Yussuf, anasema mara nyingi amekuwa akijichanganya na watu mbalimbali na kubadilishana nao mawazo na kuongeza kuwa, yuko tofauti na wasanii wengine ambao wakianza kupata mafanikio hujitenga na jamii.

"Siku zote napenda kuishi maisha ya kawaida sana sina majivuno kama wasanii wengine...muda mwingi huutumia katika shughuli za kijamii na nipo karibu sana na watu," anasema.