WAKALI wa Muziki wa Taarab hapa nchini na nje ya nchi, Jahazi Morden Taarab wamepania kuwapagawisha mashabiki na wapenzi wao katika shoo yao kabambe itakayofanyika Jumamosi ijayo pale katika ukumbi wa Travetine Hotel, Magomeni.
Akizungumza akiwa ziarani kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara Mkurugezi wa Jahazi, Mzee Yussuf alisema shoo hiyo itakuwa maalumu kwa wapenzi na mashabiki wao.
Alisema katika onyesho hilo la Vunja Jungu, wakali hao wa taarab, watasindikizwa na yale makundi maarufu ya burudani akiyazungumzia, Baikoko kutoka Tanga, Welawela na Kitu Tigo yote ya Jijini Dar es Salaam.
Mzee Yussuf alisema siku hiyo Jahazi itapiga nyimbo zake zote zinazotamba ikiwemo Wagombanao ndio wapatanao ulioimbwa na Mfalme na dada yake Hadija, Hakuna Mkamilifu- Fatma Kasimu, Tuacheni kama tulivyo- Mohamed Ally 'Mtoto pori' na Mlijua Mtasema- Hadija Yussuf.
Alisema mbali na nyimbo hizo, Jahazi itapiga nyimbo zake zote zinazotamba na zilizowahi kutamba bila kusahau ule wimbo wa msumari. Aliongeza kuwa katika onyesho hilo, mtu atakayependeza atapata zawadi na hiyo itakuwa zawadi maalumu kutoka kwa Mfalme.
Mzee Yussuf alisema kiingilio katika onyesho hilo itakuwa sh. 7000 fedha halali ya kitanzania na kuwaomba wapenzi na mashabiki wa kundi hilo kujitokeza kwa wingi siku hiyo.
Na Mudy Tela 'Mzee wa London'
0716 204548