Powered By Blogger

Monday, December 3, 2012

Mfahamu Rahma Machupa kinda wa Jahazi Morden atayemvulia kofia Mfalme Mzee Yussuf

 Rahma Machupa
Shostito Rahma akiimba

RAHMA Machupa ni muimbaji chipukizi wa taarab anayeibukia kwa kasi katika tasnia ya muziki huo hapa nchini.

Muimbaji huyo, anayetokea kwenye familia ya wanamuziki, katika siku za hivi karibuni ameonyesha uwezo mkubwa katika kundi lake la Jahazi Morden Taarab 'Wana wa nakshinakshi'.

Akizungumza na mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, Rahma anasema kipaji chake cha uimbaji  kilianza kuibuka akiwa katika shule ya sekondari ya Sinza.

Anasema  akiwa katika shule hiyo alikuwa akishiriki kuimba nyimbo mbalimbali kwa kushirikiana na wanafunzi wenzake hususan wakati wa sherehe.

Rahma, anasema mwaka 2010 baada ya kuhitimu kidato cha nne katika shule hiyo alijiunga na kundi la Mashauzi Classic chini ya Isha Mashauzi 'Jike la Simba'.

Anasema baada ya kujinga na kundi hilo na kuonyesha uwezo mkubwa, alitunga wimbo unaofahamika kama 'Sijamuona kati yenu wa kunirusha roho'

Rahma anasema wimbo huo, ulikonga vilivyo nyoyo za wapenzi wa burudani na kuanzia hapo jina lake lilianza kusikika kila kona ya mtaa.

Anasema pamoja na kuachia kibao hicho, hakufanikiwa kukaa sana kwenye kundi hilo kutokana na sababu mbalimbali na ndipo alipojiunga na Jahazi.

Muimbaji huyo mwenye umbo la wastani na sauti maridhawa, anasema baada ya kujiunga na Jahazi chini ya 'Mfalme' Mzee Yussuf aliendelea kuonyesha uwezo wake wa uimbaji.

"Kwa kweli baada ya kujiunga na Jahazi kipaji changu kimezidi kukua na kadri siku zinavyokwenda nazidi kujipatia umaarufu kwa mashabiki wangu.

"Juhudi na uwezo mkubwa nilizozionyesha katikan kundi la Jahazi ndio zimemshawishi Mzee Yussuf kunipa wimbo katika albamu yetu mpya itakayozinduliwa hivi karibuni," anasema.

Anasema kutokana na uwezo na umahiri alionyesha akiwa na kundi hilo, amekabidhiwa wimbo unaofahamika kama Nipe stara na kudai utafanya vizuri kwenye anga za burudani.

Rahma anasema wimbo huo, ni miongoni mwa nyimbo zitakazokuwemo kwenye albamu mpya ya Jahazi itakayozinduliwa mwezi ujao.

"Najiamini naweza na nitafanya kila liwezekanavyo nifanye vizuri kwenye tasnia hii ya muziki wa mwambao ili nifikie lengo nililokusudia, ninawaahidi mashabiki wangu sitowaangusha," alijigamba muimbaji huyo.

Anasema akiwa katika kundi hilo atatumia uwezo wake wote kufikia lengo lake la kuwa muimbaji bora na mwenye uwezo mkubwa kama walivyo waimbaji wengine.

Rahma, anasema binafsi anavutiwa sana na muimbaji mkongwe wa taarab hapa nchini, Rukia Ramadhani kutokana na uimbaji wake na tungo zake maridhawa.

Anasema mbali na muimbaji huyo, anavutiwa na Hadija Yussuf na Leila Rashid na kwamba anatamani siku moja awe na uwezo kama waimba hao.

Akimzungumzia Mzee Yussuf, Rahma anasema ni muimbaji mahiri asiyependa makuu na hana upendeleo ndani ya kundi lake.

Anasema Yussuf, amekuwa na mchango mkubwa kwa waimbaji wake hususan chipukizi na kwamba anawafundisha mambo mengi ya muzi na maisha.

Rahma, anasema matarajio yake ni kumiliki kundi lake la muziki na kuwa muimbaji bora ndani na nje ya nchi.

Pamoja na kuwa muimbaji bora, anaelekeza nguvu zake kwenye elimu na kwamba anafikiria kurudi darasani kuendelea na masomo mpaka afike chuo kikuu.

Muimbaji huyo, anasema amezaliwa miaka 22 iliyopita jijini Dar es Salaam na ni mtoto wa mwisho kati ya wanane katika familia yao.