Wakali wa muziki wa taarab nchini, bendi ya Jahazi Morden Taarab 'Wana wa nakshi nakshi' usiku wa kuamkia leo limekonga vilivyo nyoyo za wapenzi na mashabiki wao katika onyesho kabambe lililofanyika jana pale kata ya 14 Temeke mjini Dar es Salaam.
Katika onyesho hilo, Jahazi wakiongozwa na Mkurugenzi wa kundi hilo, Mfalme Mzee Yussuf liliporomosha burudani maridhawa na kuufanya ukumbi huo, kuripuka shangwe, vifijo na kelele za hapa na pale.
Ukumbi huo, ulifurika maelfu ya mashabiki ambapo Jahazi ilipiga vipao vyao vyote vinavyotamba na vile vilivyowahi kutamba na kusababisha mashabiki wasikali vitu vyao na muda wote kujimwaga uwanjani kuserebuka kwa furaha.
Majira ya saa 7.45 usiku, Mzee Yussuf aliwaacha hoi mashabiki waliojitokeza katika ukumbi huo, baada ya kuwaonjeshwa vibao viwili vipya vya Jahazi vinavyotarajiwa kuzinduliwa Desemba 25, mwaka huu ambapo kundi hilo litatimiza miaka mitano tangu kuzaliwa.
Katika hatua nyingine, Kundi hilo, lenye mashabiki wenye ndani na nje ya nchi limesema hivi sasa limeimariki ambapo linatarajia kupata wasanii wapya. Kundi hilo leo linatarajia kuachia show ya aina yake pale katika ukumbi wake wa nyumbani, Travetine Hoteli na Jumatano litaporomosha burudani ya nguvu katika ukumbi wa GADAFI uliopo Yombo Buza.